Rafiki Kwa Ajili Yako

Yesu Rafiki Yako

Jesus is your friend

Ninaye rafiki. Yeye ndiye rafiki bora ambaye nimewahi kujua. Yeye ni mwema sana na mkweli ambaye na wewe pia ningependa umfahamu. Jina lake ni Yesu. Cha kustajaabisha ni kwamba na yeye angependa awe rafiki yako.

Ngoja nikuambie habari zake. Tunasoma hadithi hii katika Biblia. Biblia ni kweli. Ni neno la Mungu. Mungu ndiye aliyeumba ulimwengu na vitu vyote vilivyomo. Yeye ni Bwana wa Mbinguni na dunia. Anatoa uzima na pumzi kwa viumbe vyote.

God's creation

Maandiko kamili ya: Rafiki Kwa Ajili Yako

Yesu ni Mwana wa Mungu. Alitumwa na Mungu kutoka Mbinguni kuja duniani ili awe Mwokozi wetu. Mungu aliupenda ulimwengu sana (inamaanisha alikupenda wewe na mimi) hata akamtoa Mwanawe pekee, Yesu, (afe kwa ajili ya dhambi zetu) ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. (Yohana 3:16)

Yesu alikuja duniani kama mtoto mchanga. Baba na Mama yake wa hapa duniani walikuwa Yosefu na Maria. Alizaliwa katika zizi na kulazwa horini.

Jesus' birth

Yesu alikulia nyumbani kwa Yosefu na Maria, na aliwatii. Alikuwa na ndugu na dada wa kucheza nao. Alimsaidia Yosefu katika kazi yake ya useremala.

Jesus and the lad with food

Yesu alipokuwa mtu mzima, aliwafundisha watu habari ya Baba yake wa Mbinguni. Aliwaonyesha upendo wa Mungu kwao. Aliwaponya wagonjwa na kuwafariji waliokuwa kwenye taabu. Alikuwa Rafiki ya watoto. Aliwakaribisha wasogee karibu naye. Alikuwa na muda kwa hao wadogo. Watoto walimpenda Yesu, na walipenda kuwa pamoja naye.

Baadhi ya watu hawakumpenda Yesu. Walimwonea wivu na hata kumchukia. Walimchukia sana, hata walitaka kumwua. Siku moja ya kutisha walimwua Yesu kwa kumpigilia misumari msalabani. Yesu hakufanya makosa. Ilimlazimu afe badala yetu kwa sababu wewe na mimi tumefanya makosa.

Jesus on the cross

Hadithi ya Yesu haikomei pale penye kifo chake. Mungu alimfufua kutoka wafu! Wafuasi wake walimwona. Kisha siku moja alirudi mbinguni.

Leo anaweza kukuona na kukusikia. Yeye hujua yote juu yako na anakujali. Umwendee tu katika sala.

Mwambie shida zako zote. Yuko tayari kukusaidia. Unaweza kuongea naye kwa maombi, wakati wowote, popote pale.

 Kuna siku atarudi tena! Wote wanaomwamini atawapeleka nyumbani, Mbinguni.

Jesus listening to a woman pray

( swahili kiswahili )

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Maisha Yako Yameandikwa

Biblia hutuambia kwamba Mungu anajua kila kitu, na kwamba anahifadhi maandishi ya maisha yetu. Tutahitajika kutoa maelezo ya aliyoandika siku ya hukumu (Warumi 14:11-12). “Na niliwaona wafu, wadogo kwa wakubwa wamesimama mbele ya Mungu; na vitabu vilifunguliwa: na kitabu kingine cha uzima kikafunguliwa, na wafu walihukumiwa kwa yale yaliyoandikwa katika vitabu kulingana na kazi zao” (Ufunuo 20:12).  Tutakaposimama katika hukumu mbele ya Mungu, tutakuwa tumechelewa kubadili maisha yetu wala mwisho wetu wa milele.

Mungu huona yote, mema na maovu tunayoyafanya. Yeye hufahamu msimamo wetu halisi na mawazo yetu--- ikiwa mema au maovu. “Wala hakuna kiumbe chochote kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote ni utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu” (Waebrania 4:13). Tutahukumiwa kwa orodha ya matendo yetu. “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya” (Mhubiri 12:14).

CHAGUO NI LETU

Katika uhai huu tunaweza kuchagua kumfuata Kristo na mafundisho yake au kufuata tamaa ya mwili wetu unaopenda dhambi. Biblia ina orodha ya dhambi za mwili katika Wagalatia sura ya 5. Ndiyo haya, “Uasherati, uzinzi, uchafu, ufisadi, kuabudu sanamu, uchawi, ugomvi,wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo” (Wagalatia 5: 19-21). Ikiwa baadhi ya haya yamepatikana kwetu, andiko hili hutuambia kwamba hatuwezi kuurithi ufalme wa Mungu. Kwa neema ya Baba wa Mbinguni aliye na upendo, tukitubu na kumwamini Kristo, tunapata msamaha. Kisha damu ya Kristo hufunika dhambi na zinafutwa kwenye orodha.

Pia Biblia inayo orodha ya matunda yanayozalishwa katika maisha yetu tunapojitoa kwa Mungu. “Lakini matunda ya roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utulivu, wema, imani, upole, kiasi…..” (Wagalatia 5:22-23). Ni muujiza wa neema kuwa na matunda haya pamoja na majina yetu kuandikwa Mbinguni.

Maandiko kamili ya: Maisha Yako Yameandikwa

Neno la Mungu hutuonya juu ya mtego na hatari ambayo inatukabili. “Pia jueni hili, kwamba katika siku za mwisho nyakati za hatari zitatokea. Kwa maana watu watajipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna, wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu, wenye mfano wa utauwa, lakini wakikana nguvu zake; hao nao ujiepushe nao” (2Tim 3:15). Ni dhahiri kwamba hali zilizo katika ulimwengu hazifai maisha ya ukristo. Tumezungukwa na uovu wa kila namna ya ulaghai. Kwa kuwa tunawajibika kwa kila neno na tendo letu, tunapaswa kufanya chaguzi ambazo zitazalisha matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha yetu.

Katika Biblia kuna mafungu mengi yanayotuonya kuhusu kutokujali wokovu wetu. “Na kama wenye haki hawaokolewi, Je, watakuwaje wenye dhambi na wasiomcha Mungu?” (1Petro 4:18).  “Na Bwana alimwambia Musa, yeyote anitendaye dhambi, nitafuta jina lake katika kitabu changu” (Kutoka 32:33). “Njooni mmtazame mtu (Yesu) aliyeniambia yote niliyoyatenda” (Yohana 4:29). Ingawa maneno haya ni yenye uzito Mungu ameahidi kutusamehe dhambi kama tumeamini na kutubu katika damu ya Kristo ya kulipia deni. Atazifuta dhambi zetu badala ya kufuta majina yetu kutoka kwenye orodha.

JE, JINA LAKO LIPO KATIKA KITABU CHA UZIMA?

Ili majina yetu yaandikwe katika kitabu cha uzima, ni lazima tuukubali mwaliko wa Yesu: “Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao, na kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha” (Mathayo 11:28). Hakuna anayesamehewa hatia ya dhambi pasipo damu ya Yesu. Yeye kwa sababu ya upendo, alimwaga damu yake kwa hiari juu ya msalaba kwa ajili ya dhambi zetu. Yesu alimwambia Nikodemo, “Mtu asipozaliwa kwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu” (Yohana 3:3). Pia alisema, “Msipoongoka na kuwa kama watoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Mathayo 18:3). Yesu huwaalika kila mmoja kuja kwake na kuokolewa.

Baada ya majina yetu kuandikwa katika kitabu cha uzima tusitake yafutwe tena. Yesu asema, “Tazama, naja upesi: Shika sana ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako” (Ufunuo 3:11). Na tena, “Kesheni mkiomba, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu” (Mathayo 26:41). Maandiko haya yanatuonya kuwa wanaokesha na siyo kuacha ahadi yetu ya kumtumikia Mungu. Shetani, adui wa nafsi zetu, ameelezwa kama simba angurumae, ambaye ataturarua tusipompinga kwa kuwa imara kwenye imani. (1Petro 5:8-9) Tunapaswa kulichunguza Neno la Mungu na kuwa thabiti katika sala zetu, la sivyo wokovu wetu utatuteleza. Tumeahidiwa, “Yeye ashindaye atavikwa hivyo mavazi meupe, na sitaondoa jina lake katika kitabu cha uzima, lakini nitakiri jina lake mbele ya Baba yangu, na mbele ya malaika zake” (Ufunuo 3:5).

KUWA TAYARI KWA SIKU YA HUKUMU

Leo ndiyo siku ya neema, ni nafasi ya kutengeneza nyumba yetu na kujiandaa kwa siku ya hukumu. Tukifa miili yetu inayokufa itarudi mavumbini. Lakini atakaporudi Yesu kuuhukumu ulimwengu siku ya ufufuo, kila mmoja atapokea mwili usiokufa ambao utakaa milele mbinguni au motoni. Kama kuna doa la dhambi mioyoni mwetu, tumgeukie Yesu LEO aisafishe, kisha twaweza kuwa tayari kuingia mbinguni siku hiyo kuu. “Na hakitaingia mle kilicho najisi, wala afanyaye machukizo, wala mwongo: bali wale walioandikiwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo” (Ufunuo 21:27).

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi

Jibu Kwa Ajili Yako

Jesus at the well

Je, wajua kwamba kuna mtu ambaye hujua yote juu yako? Ni Mungu aliyeumba ulimwengu na vitu vyote vilivyomo. Yesu, Mwana wa Mungu, pia hujua yote ambayo umeshafanya. Yeye hujua yaliyopita, ya leo, na yajayo. Yeye anakupenda na alikuja ulimwenguni kukuokoa kutoka dhambini.  Anao mpango wa uzima wako ili kukuletea furaha.

Siku moja Yesu alikuwa akitembea na rafiki zake alienda katika kijiji cha Samaria. Yesu alikaa kando ya kisima wakati rafiki zake walienda kununua chakula.

Yesu alipokuwa amekaa pale, mwanamke mmoja alikuja kuchota maji kisimani. Yesu alimwambia, “Naomba unipe maji ninywe.”

Maandiko kamili ya: Jibu Kwa Ajili Yako

Mwanamke alishangaa, akasema, “Je, unaniomba maji unywe? Je, kwani hujui mimi ni Msamaria, na ninyi Wayahudi hamna uhusiano nasi?”

Kwa upole Yesu alijibu, “Kama kwa hakika ungemjua Mungu, na ni nani anayeongea nawe, ungeniomba Mimi nikupe maji ya uzima, na ningeshafanya kwa furaha.”

Mwanamke huyo alimtazama kwa mshangao, akasema, “Bwana, kisima ni kirefu, Je, utachotaje maji ya uzima na huna chombo?”

The woman running to town

Yesu akajibu tena, “Wale wanaokunywa maji ya kisima hiki, watapata kiu tena, lakini ukinywa maji ninayoweza kutoa, kamwe hutapata kiu tena.”

Mwanamke huyo alisema, “Bwana, nipe maji hayo ili nisipate kiu tena, wala nisihitaji kurudi kuchota maji hapa.”

Yesu alimwambia, “Nenda umwambie mume wako na uje naye hapa.”

Alijibu, “Sina mume.”

Yesu alisema, “Ni kweli. Umeshakuwa na wanamume watano, lakini mmoja unaye sasa siye mume wako”.

Yule dada alijiuliza akistaajabu,  Mtu huyu anajuaje habari zangu? “Bwana, ninaweza kuona kwamba wewe ni nabii. Watu wangu walimwabudu Mungu mahali hapa hapa, ninyi mnasema kwamba Yerusalemu ndiyo mahali ya ibada.”

Yesu alimwambia, “Hakuna mahali muhimu twaweza kumwabudu, waumini wa kweli leo wanaweza kumwabudu Baba katika Roho na kweli popote.”

Mwanamke yule alisema, “Najua kwamba Masihi, aitwaye Kristo, anakuja, na atakapokuja, atatuelezea yote.”

Kisha Yesu alimwambia kwa uwazi, “Ndiye Mimi.”

Basi yule dada aliacha mtungi wake wa maji akarudi mjini. Aliita, “Njooni! Njooni na kumwona mtu ambaye ameniambia mambo yote niliyowahi kutenda. Je, yeye siye Kristo?”

Kisha watu wakatoka mjini kumlaki Yesu. Wengi waliamini kwamba yeye ndiye Kristo Mwokozi, kwa sababu alijua habari zao zote. Unaweza kusoma habari hii katika Biblia, katika Injili ya Mtakatifu Yohana 4:3-42.

Jesus teaching the crowd

Yesu hujua habari zetu zote, mema pamoja na mabaya. Tungependa kuficha mabaya ambayo tumetenda katika maisha yetu, lakini hatuwezi kumficha Yesu. Amekuja kutuokoa kutoka kwenye adhabu tunayostahili kwa kufanya uovu. Anaweza kuondoa mzigo mzito ule unaohisi katika moyo wako, na kukupa amani. Alikufa ili aondoe dhambi zako na kwamba akufanyie uwezekano wa kwenda mbinguni utakapofariki.

Yesu ndiye jibu la maswali yako yote, na mahitaji yako yote. Yeye anataka awe rafiki yako. Anatamani ajaze moyo ulio tupu. Anaweza kubadilisha wasiwasi na hofu yako kwa amani na utulivu.

Yesu husema, “Njooni Kwangu….. na nitawapumzisha.” (Mathayo 11:28) Mwombe tu Mungu, na mwambie una huzuni kwa ajili ya dhambi zako. Mwombe Yesu aje katika maisha yako. Unapomkabidhi Mungu Mkuu huyu binafsi yako kwa imani, atakaa moyoni mwako. Na uwepo wake utakupa shangwe. Atakufanya uwe na lengo lenye maana, uwe na makusudi, na uwe na nguvu katika maisha yako. Atakuwa jibu kwa ajili yako.

Mawasiliano

Kuagiza Vipeperushi